Majeruhi
Na Igenga Mtatiro, Tarime
Hii siyo siasa! Ndivyo walivyokuwa wakisema watu wengi mjini hapa baada ya hivi karibuni kushuhudia mtu mmoja, Mwita Bhoke Watei (37), mkazi wa Kijiji cha Nyandage, Kata ya Nyanungu, Tarime mkoani hapa, akiuawa kwa kukatwa mapanga katika vurugu za kampeni za uchaguzi zinazoendelea nchini kote kwa sasa.
Mmoja wa mashuhuda hao, Pius Londo, mkazi wa wilayani hapa aliliambia Uwazi kuwa siasa safi ni zile ambazo hazihusishi vurugu na kwamba katika kipindi tulichonacho Watanzania wanahitaji siasa za kistaarabu.
Naye Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Tarime na Rorya, ACP Lazaro Mambosasa amekemea vikali matukio hayo huku akifafanua kuwa, pia kulikuwa na watu watano waliojeruhiwa kwenye vurugu hizo zisizo za kistaarabu.
Baadhi ya majeruhi
Aliwataja waliojeruhiwa vibaya kwa kukatwa mapanga, visu na kupigwa na mawe katika eneo la Mangucha kuwa ni pamoja na Chacha Mwita Chacha (32), mkazi wa Nyandage aliyejeruhiwa mgongoni, miguuni na mikononi wakati Kimunye Chacha Mogesi (54), mkazi wa Kegonga alijeruhiwa mikono na kichwani huku Elizabert William Marwa (43) akijeruhiwa sehemu mbalimbali mwilini.
Kamanda Mambosasa aliwataja wengine waliojeruhiwa sehemu mbambali wilayani hapa katika vurugu za kampeni kuwa ni Queen Ryoba (47), mfanyabiashara aliyeumizwa sehemu mbalimbali za mwili wake na Nyaitati Maranya (30), mkazi wa Kegonga alijeruhiwa mikono.
Kamanda huyo wa polisi alibainisha kuwa chanzo cha vurugu hizo katika kampeni ni wafuasi wa chama kimoja walipokuwa wakiandamana kumpokea mgombea udiwani wao ndipo wakakutana na wa chama kingine na kuanza vurugu.
Naye Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Rose Hosea aliliambia gazeti hili kuwa walipokea mwili wa marehemu huyo aliyekuwa amefariki dunia baada ya kuumizwa vibaya kisha wakapokea majeruhi kadhaa.