ULE msemo usemao ‘wagombanao ndiyo wapatanao’ umetimia kwa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ baada ya kuwa na mgogoro kwa muda mrefu na baba yake, Abdul Jumaa ‘Baba D’ ambapo anadaiwa kusalimu amri na sasa wanaelewana, Risasi Jumamosi linakuwa la kwanza kukunyetishia.

TUJIUNGEA NA CHANZO

Chanzo makini ambacho ni rafiki wa karibu wa Baba D, mapema wiki hii kililieleza gazeti hili kwamba, kwa sasa Diamond amesalimu amri kwa baba yake kwani amekuwa akimsikiliza na kumsaidia pale anapokuwa na shida tofauti na ilivyokuwa awali.

“Angalau sasa Diamond anamsaidia baba yake kwani hata akimpigia simu anamsikiliza na anampa fedha ndogondogo za matumizi tofauti na zamani,” kilinyetisha chanzo hicho kwa sharti kuu moja tu la kutochorwa jina gazetini.


NYUMBANI KWA BABA D

Baada ya kupata ‘news’ hizo, gazeti hili lilimfungia safari baba Diamond hadi nyumbani kwake, Magomeni jijini Dar ambapo alikiri kwamba mwanaye Diamond kwa sasa anamsikiliza na hata akiwa na shida anamsaidia japokuwa bado anasumbuliwa na mguu na anahitaji matibabu ya kina zaidi kwani inatoa maji na kuvimba.

SHUKRANI KWA GLOBAL

“Nawashukuru hata ninyi Magazeti ya Global kwani mmechangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya mwanangu. Kwa sasa ananisadia hata nikimpigia simu ananisikiliza tofauti na zamani,” alisema baba Diamond.

BABA D ATOA NENO


Mzazi huyo wa staa wa Ngoma ya Nana alikwenda mbele zaidi na kumtaka mwanaye Diamond alete heshima kwa familia kwa kuoa kama ameamua kuwa na Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambaye kwa sasa ana ujauzito wake.

Baba D alimtaka mwanaye huyo afunge ndoa na Zari kihalali kwani kila kunapokucha wanawake wazuri wanazaliwa, asije akaishia kuvishavisha wanawake pete za uchumba tu bila kuoa.

“Diamond amepata fedha akiwa kijana, ni bahati iliyoje hiyo! Anatakiwa sasa atulie na mwanamke mmoja kama amemchagua Zari basi wafunge ndoa halali maana baadhi ya wanaume huwa tuna tabia moja, kwamba, mwanamke akishazaa tunamuona mvuto wake umeisha.

“Hivyo, hata kwa Diamond inaweza kutokea baada ya Zari kujifungua, akamuona hivyo na akakutana na mwanamke mwingine mzuri ambaye hajazaa, akaamua kuwa naye tena na kumsahau huyo (Zari) lakini akiwa kwenye ndoa ni afadhali,” alisema baba Diamond.


AMKUMBUKA WEMA

Hata hivyo, katika mazungumzo hayo maalum, baba Diamond alimkumbuka aliyekuwa mpenzi wa mwanaye, Wema Sepetu kwamba ni mwanamke mzuri na anayefaa japokuwa mwanaye ameamua kuwa na Zari ambaye pia ni mzuri ila anamkumbuka sana Wema kwani ndiye aliyewahi kutambulishwa na akawa anamjali.

DIAMOND AENDELEA KUTISHA NIGERIA

Baada ya kusikia upande wa baba, gazeti hili lilimtafuta Diamond ili kuthibitisha ishu hiyo ambapo alijibu kwa kifupi kuwa yupo Nigeria akiendelea na kampeni ya kuomba kupigiwa kura kwenye Tuzo za MTV-Mama’s.

HUKO NYUMA

Diamond na baba yake walikuwa kwenye mgogoro wa muda mrefu ambapo mzazi huyo alikuwa akilalamika kwamba mwanaye huyo hakuwa akimjali na hata alipokuwa akijaribu kumpigia simu alikuwa hampi ushirikiano.
GPL
 
Top